Jeshi la Zimbabwe limesoma taarifa kwenye kituo cha runinga cha
serikali ZBC, likisema kuwa linachukua hatua ya kuwalenga wahalifu.
Hata hivyo limesema kuwa hayo sio mapinduzi ya kijeshi na Rais
Mugabe yuko salama.
Milio mikubwa ya risasi ilisikika katika maeneo ya kaskazini mwa
mji mkuu Harare mapema leo.
Taarifa hiyo ya jeshi ilikuja saa kadhaa baada ya jeshi
kudhibiti kituo cha ZBC.
Mwanamume mmoja ambaye alikuwa amevaa sare za jeshi alisema kuwa
jeshi linataka kukabiliana na watu ambao wanatenda uhalifu unaoleta madhara ya
kijamii na kiuchumi nchini Zimbabwe.
"Wakati tutakapomalzia wajibu wetu, tunatarajia kuwa hali
itadudi kuwa sawa."
Taarifa hiyo ilisema kuwa Mugabe 93, na familia yake wako
salama. Harare
Haijulikani ni nani anaongoza hatua hiyo ya kijeshi.
Magari ya wanajeshi waliojihami kwa silaha yameonekana maeneo ya
mjini Harare.
Hali hiyo ya wasi wasi wa lolote kuweza kutokea, imeanza hapo
jana jioni, ambapo wanajeshi wakiwa na silaha walionekana wakijipanga katika
maeneo kadhaa pamoja na kuzingira ofisi za shirika la utangazaji la Zimbabwe
ZBC.
Hata hivyo taarifa zinasema kuwa wafanyakazi wa shirika hilo la
utangazaji ZBC, waliambiwa na wanajeshi hao kwamba hawapaswi kuwa na wasiwasi
na kwamba uwepo wa vikosi hivyo ni kwa lengo la kulinda eneo hilo.
Milipuko mizito imeendelea kusikika pia.
Chama tawala nchini Zimbabwe kimemtuhumu mkuu wa majeshi
Constantino Chiwenga, kwa hatua yake ya madai kuwa jeshi lipo tayari kuingilia
mzozo huo wa kisiasa kwa lengo la kulinda wapigania uhuru wa taifa hilo.
Hakuna kauli yoyote iliyotolewa na Rais Robert Mugabe kutokana
na hali ya sasa nchini mwake.
Marekani imesema kuwa inafuatilia kwa karibu hali ya Zimbabwe na
kutoa rai pande zote kutatua mzozo huo kwa njia ya amani.
Naye Balozi wa Marekani nchini Zimbabwe kupitia ukurasa wake wa
Tiwtter amesema kuwa leo watasitisha shughuli za kiofisi ubalozini hapo
kutokana na halisi ya sasa mjini Harare.
Balozi wa Zimbabwe nchini Afrika Kusini Isack Moyo ameliambia
shirika la habari la Reuters kuwa serikali ipo imara katika jambo hilo na
kuzuia uwezekano wowote wa kufanyika kwa mapinduzi.
SOURCE. BBCSWAHILI.COM


0 Maoni