NA.MWANDISHI WETU.
Mkuu wa Mkoa wa Manyara,Alexander Mnyeti amemuagiza mkuu wawilaya ya Kiteto,Mhandisi Tumaini Magessa kumkamata mbunge wa Kiteto (CCM),
Emmanuel Papian endapo atabainika kuwa anachochea migogoro ya ardhi.
Mnyeti amesema hayo
Ijumaa Januari 19, 2018 wakati akihitimisha ziara yake ya siku saba
alipotembelea wilaya ya Kiteto.
Amesema endapo Papian
anasababisha migogoro ya ardhi kwa kuchochea wananchi walime kwenye hifadhi,
anapaswa kuchukuliwa hatua.
“Mkuu wa wilaya wewe
ndiye mteule wa Rais kwenye eneo hili la Kiteto. Endapo mtu mwingine hata kama
ni mbunge wa jimbo akiwa anachochea migogoro ya ardhi, uwe unawakamata na
kuwaweka ndani,” amesema Mnyeti.
Amesema migogoro ya
ardhi kwenye wilaya ya Kiteto haitaweza kumalizika endapo wanasiasa wataendelea
kuwachonganisha wakulima na wafugaji.
“Mbunge asiote mapembe
na kupanda kichwani kwako, wewe ndiye mtawala wa hapa. Nataka siku nyingine
unipigie simu kuwa umemkamata na kumweka ndani mbunge ili asirudie hilo,” amesema
Mnyeti na kuongeza,
“Mkuu wa wilaya
unapozungumzia mgogoro wa kijiji zungumza sehemu husika na kama mbunge
akiendelea kuchochea umkamate,” amesema Mnyeti.
Akizungumza kwa njia
ya simu na Mwananchi, Papian hakukubali wala kukataa juu ya yeye kuchochea na
kusababisha migogoro ya ardhi, ila amesema muda utaongea.
“Hapa tunavyozungumza
nipo kwenye gari, ila suala hilo uliloniuliza litajulikana huko mbeleni
tunakokwenda hivyo tujipe muda tuu itabainika,” amesema Papian.
SOURCE.MWANANCHI


0 Maoni